Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba amekutana kwa mazungumzo na Mbunge wa Bunge la Uturuki na Mwenyekiti wa Umoja wa Urafiki wa Wabunge wa Tanzania na nchi hiyo, Mhe. Zeki Korkutata

Katika mazungumzo yao ambayo yamefanyika tarehe 16 Aprili 2024 jijini Ankara, ikiwa ni sehemu ya kukamilisha maandalizi ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayotarajiwa kufanyika nchini humo kuanzia tarehe 17 hadi 21 Aprili 2024 viongozi hao wamejadili maeneo muhimu ya ushirikiano ambayo pia yatajadiliwa kwa uzito wa juu wakati wa ziara hiyo.

Mhe. Makamba amesema miongoni mwa masuala muhimu nchi hizi mbili zitayapa kipaumbele kupitia ziara hii, ni pamoja na kufanyika haraka kwa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kwenye masuala ya Uchumi baina ya Tanzania na Uturuki.

Amesema kupitia tume hii nchi hizi mbili zitapata fursa ya kujadili kwa kina sekta za ushirikiano wa kimkakati baina yake na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa makubaliano yote yatakayofikiwa wakati wa ziara hii ya kihistoria.

  • Mhe. Korkutata naye akizungumza. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Bakari na kulia ni Mkalimani wa Mhe. Korkutata
  • Mkutano ukiendelea