Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amefanya ziara ya kikazi nchini Uturuki, tarehe 4-6 Juni 2026, ambapo alishiriki kikao cha mawaziri kilichofanyika Jijini Istanbul, Juni 5, 2026, kilichohudhuriwa na mawaziri wa sekta za viwanda, biashara, teknolojia kutoka mataifa mbalimbali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na sekta binafsi.

Kikao hicho kiliangazia mageuzi ya kijani katika sekta ya viwanda na jitihada za kufikia azma ya taka sifuri ili kuimarisha matumizi endelevu ya malighafi, kudhibiti uzalishaji wa taka na kuongeza thamani ya bidhaa

Kupitia kikao hicho Waziri Kapinga ameeleza jitihada mbambali ambazo zimechukuliwa na Tanzania katika kuimarisha sekta ya viwanda kwa kuzingatia matumizi bora ya rasilimali na uhifadhi wa mazingira. Ameeleza kuwa taka sifuri na uchumi rejeshi ni fursa kwa nchi zinazoendelea kupitia matumizi endelevu ya malighafi, kudhibiti uzalishaji wa taka na kuongeza thamani ya bidhaa.

Vilevile, Waziri Kapinga amebainisha kwamba maendeleo ya mageuzi ya kijani yanahitaji uwekezaji katika miundombinu, teknolojia na pamoja na ushirikiano thabiti miongoni mwa mataifa duniani.

Hivyo, alitoa rai kwa nchi zinazoendelea kupewa kipaumbele katika upatikanaji wa teknolojia, utaalamu, rasilimali fedha na ubunifu utakaosaida kukuza sekta ya viwanda. Vilevile, alieleza dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa na wadau wa maendeleo katika kuendeleza viwanda vinavyozingatia matumizi bora ya rasilimali na kulinda mazingira ili kujenga uchumi imara, jumuishi na endelevu.