Mazungumzo kati ya Waziri Judith Kapinga na Waziri wa Biashara wa Uturuki, Mhe. Prof. Dkt. Ömer Bolat, yaliyofanyika Juni 06, 2026, Istanbul, yalilenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kuvutia uwekezaji hasa katika maeneo ya kimkakati ili kuongeza urari wa biashara na kufungua fursa zaidi kiuchumi kati ya Tanzania na Uturuki.
Biashara baina ya nchi hizi mbili imefikia Dola za Marekani milioni 354 kwa mwaka 2026, huku kukiwa na lengo la kufikia Dola za Marekani bilioni moja.
Mawaziri hao walijadili azma ya kuimarisha mazingira wezeshi ili kuvutia zaidi wafanyabiashara na sekta binafsi baina ya pande mbili kutekeleza shughuli zao kwa ufanisi.
Aidha, waliafiki kufanya Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Biashara Kati ya Tanzania na Uturuki unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwaka 2026. Mkutano huo utatoa fursa ya kujadili kwa kina ushirikiano wa kibiashara wenye maslahi ya pande zote mbili.
Waziri Kapinga alitumia fursa ya mazungumzo hayo kuelezea utayari wa Tanzania kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika sekta ya biashara. Tanzania imewaalika wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchini humo kuja nchini kutumia fursa zilizopo.
Kadhalika, Waziri Bolat alieleza kwamba Uturuki iko tayari kuendelea kukuza ushirikiano na Tanzania kwa maendeleo ya nchi zote mbili. Katika eneo hili alitaja hatua ya kusainiwa kwa mkataba wa kuondoa utozaji kodi mara mbili kati ya Tanzania na Uturuki mwezi Mei 2026, ambao unachochea biashara na kuvutia uwekezaji.
Tanzania na Uturuki ni washirika wa kimkakati katika maeneo mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji, teknolojia na maendeleo ya ujuzi ambapo nchi hizi mbili zina dhamira ya dhati ya kuimarisha uhusiano uliopo kwa maslahi ya pande zote.

