Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Zana za Kilimo na Matumizi ya Nishati Mbadala kutoka Wizara ya kilimo, Mhandisi Henry Godrey Kilapilo umeshiriki maonesho ya Kilimo ya Konya (Konya Agriculture Fair) yaliyofanyika Konya, Uturuki kuanzia tarehe 07 hadi 11 Aprili, 2026.

Ujumbe huo ukiwa nchini Uturuki ulipata fursa ya kuzungumza na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo, Mhe. Iddi Seif Bakari kuhusu maonesho hayo.

Balozi Bakari alieleza kuwa maonesho hayo ni fursa kwa Tanzania kuimarisha ushirikiano na wadau wa kilimo ikiwemo kampuni na taasisi zilizoshiriki katika kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo,  kujifunza shughuli za kilimo, matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuanzisha ubia wa pamoja na kampuni kutoka nchini Uturuki ili kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo.