Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uturuki zimesaini maazimio ya kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa manufaa ya mataifa hayo mawili.

Maazimio hayo yamesainiwa tarehe 5 Mei 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kusini mwa Afrika na Ushrikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, Balozi Volkan Işıkcı, alisaini kwa niaba ya Jamhuri ya Uturuki.

Akizungumza katika kikao na Waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa kikao hicho, Balozi Mussa alisema Tanzania na Uturuki zimehitimisha kwa mafanikio makubwa Kikao cha Kwanza cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano, kilichofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 4 hadi 5 Mei 2026.

“Kukamilika kwa kikao hiki kunafungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki, ambao umedumu kwa zaidi ya miongo sita sasa, na kuwawezesha mataifa haya kuendelea kuibua fursa za kimkakati za ushirikiano na kuzitekeleza kwa wakati kwa manufaa ya mataifa yote mawili,” alifafanua Balozi Mussa.

Amewakaribisha wawekezaji wa Uturuki kuwekeza nchini hususan katika sekta za kiuchumi ikiwemo viwanda, kilimo, utalii na usafiri wa anga, reli, utalii, huku pande zote zikisisitiza umuhimu wa kuibua fursa mpya za kiuchumi, katika masuala ya fedha, sekta za umma na binafsi.

Balozi Mussa pia aliwataarifu Wanahabari kuwa mataifa hayo yamekubaliana Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa ujao wa Tume ya Pamoja ya Biashara, utakaofanyika katika Jijini Ankara, Uturuki.

Naye Balozi Volkan Işıkcı ameeleza azma ya Serikali ya Uturuki ya kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo za Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Uturuki (TİKA), na ameipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kulinda amani, usalama na umoja wa kitaifa, hatua inayovutia wawekezaji kutoka pande mbalimbali za dunia.

  • Balozi Said Shaib Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi Volkan Işikçi, Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki mara baada ya kusaini Maazimio ya Ushirikiano baina ya pande mbili.Balozi Said Shaib Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Balozi Volkan Işikçi, Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki mara baada ya kusaini Maazimio ya Ushirikiano baina ya pande mbili.
  • Balozi Said Shaib Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiwa pamoja na Balozi Volkan Işikçi, Mkurugenzi Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, wakati wa Mkutano wa kwanza wa Majadiliano ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mei 4-5, 2026. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mhe. Iddi Seif Bakari, Balozi wa Tanzania nchini Uturuki na Mhe. Dkt. Bekir Gezer, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania.
  • Balozi Said Shaib Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akiteta jambo na Balozi Volkan Işikçi, Mkurugenzi Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki na Mwenyekiti Mwenza (Co-Chair) wakati Mkurugenzi huyo alipofanya ziara ya kikazi nchini Tanzania mwezi Mei 2026.