Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari, amefanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho la Kimataifa la Uwekezaji na Biashara (ULUSKON), jijini Ankara, Oktoba 15, 2026. Mwenyekiti huyo aliambatana na Bw. Kemal Gürel mwanachama wa Shirikisho la ULUSKON na Mkurugenzi wa Kampuni ya Solares Renewable Energy Incorporation inayojishughulisha na masuala ya nishati jadidifu nchini Uturuki.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kukuza biashara na kufungua fursa za uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki. Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilijadili umuhimu wa kuanzisha ushirikiano katika sekta mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa nishati jadidifu na ununuzi wa zao la kahawa. Taasisi hiyo ilieleza dhamira yake ya kuhamasisha wanachama wake kutembelea na kuwekeza Tanzania ili kunufaika na soko la ndani na la kikanda, ikiwemo EAC na SADC.

Balozi Bakari aliupongeza Ujumbe wa ULUSKON na kuuhakikishia ushirikiano wa dhati katika kutekeleza shughuli zake nchini Tanzania katika miradi ya nishati jadidifu na biashara ya kahawa. Vilevile, aliwakaribisha wanachama wake kushirikiana na sekta binafsi ya Tanzania kuweka mikakati ya ushirikiano inayolenga kukuza biashara na kuvutia uwekezaji wenye maslahi kwa pande zote mbili.