Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) na Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda cha Uturuki (MÜSİAD) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa lengo la kukuza uwekezaji, kupanua masoko ya bidhaa na kufungua fursa mpya za biashara kati ya Tanzania na Uturuki.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha wawakilishi wa taasisi hizo mbili Jijini Dar es Salaam kilicholenga kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo.
Ujumbe wa TNCC uliongozwa na Bw. Leonard Masai, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, huku ujumbe wa MÜSİAD ukiongozwa na Bw. Selim Başdemir. Kikao hicho kiliandaliwa kwa uratibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki.
Katika kikao hicho, pande hizo zilikubaliana kushirikiana katika kuratibu shughuli mbalimbali za biashara na uwekezaji, zikiwemo ziara za kibiashara, utafiti wa masoko, kubadilishana taarifa za fursa za uwekezaji pamoja na kukuza ubunifu.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki kutambua fursa zilizopo katika masoko ya nchi hizo, kuanzisha mahusiano ya kibiashara na kuchochea uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
Hatua hiyo pia inaendana na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kukuza uchumi kupitia ushiriki wa sekta binafsi, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, na kuimarisha ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.



