Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari na Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda Uturuki (MÜSİAD), Ndg. Burhan Özdemir wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele ikiwemo sekta za viwanda na uzalishaji, nishati na madini, miundombinu na ujenzi, pamoja na sekta ya utalii, huku lengo likiwa ni kuongeza miradi ya uwekezaji na kukuza biashara ya pande mbili.

Wawili hao walifikia makubaliano hayo katika mazungumzo yaliyofanyika Septemba 08, 2026 jijini Istanbul, Uturuki.

Balozi Bakari amebainisha kwamba Tanzania ina fursa ya soko kubwa ndani na kikanda, ikiwemo EAC, SADC na AfCFTA yenye watu zaidi ya bilioni 1.4.

Pia, Tanzania imeboresha mazingira wezeshi kwa uwekezaji, kama vile ardhi, vivutio vya kodi, na utaratibu wa kituo kimoja cha huduma kwa wawekezaji.

Kwa upande wa Rais wa MÜSİAD, ameshukuru kwa nafasi ya mazungumzo na kueleza kwamba Jumuiya hiyo imejidhatiti kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania kupitia fursa za kimkakati na ziara rasmi kwa maslahi ya pande zote mbili.

Balozi Bakari ameipongeza MÜSİAD kwa dhamira yake ya kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania mwezi Oktoba 2026 ili kuanzisha mazungumzo rasmi na taasisi za serikali na sekta binafsi yenye lengo la kufanikisha azma ya uwekezaji. Ziara hiyo itaongozwa na Rais wa Jumuiya na itajumuisha wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali.