Tanzania na Uturuki zimeendelea kuweka msingi wa kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji na biashara kupitia fursa za kimkakati zinazolenga kukuza viwanda, kuongeza ajira na kupanua masoko ya bidhaa kati ya nchi hizi mbili.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kikao cha kimkakati kati ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Uturuki (MÜSİAD), kilichofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 15, 2026, kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Uturuki na kupanua wigo wa biashara baina ya mataifa hayo.
Ujumbe wa TISEZA uliongozwa na Bw. Daudi Riganda, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, huku ujumbe wa MÜSİAD ukiongozwa na Makamu wa Rais wa jumuiya hiyo, Bw. Selim Başdemir. Mazungumzo hayo yalilenga kuunganisha wawekezaji wa Uturuki na fursa zilizopo nchini Tanzania kupitia maeneo maalum ya kiuchumi na kongani za viwanda.
Katika kikao hicho, pande hizo zilijadili fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo na uongezaji thamani wa mazao, viwanda na uzalishaji, nishati, madini, miundombinu, ujenzi na utalii. Sekta hizo zina nafasi muhimu katika kuongeza uzalishaji, kukuza uchumi na kuimarisha biashara baina ya nchi hizi mbili.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Riganda aliukaribisha ujumbe wa MÜSİAD kutembelea maeneo maalum ya kiuchumi na kongani za viwanda ili kujionea fursa zilizopo na kutathmini uwezekano wa kuanzisha miradi ya uwekezaji nchini.
Kwa upande wake, ujumbe wa MÜSİAD ulieleza utayari wa kuendelea kuchunguza fursa zilizowasilishwa, hatua itakayosaidia kufanya maamuzi ya uwekezaji baada ya kukamilisha uchambuzi wa miradi husika.
Ushirikiano huo unatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa kuhamasisha mitaji ya Uturuki kuingia Tanzania, kuchochea maendeleo ya viwanda, kuongeza ajira na kupanua biashara ya bidhaa kati ya nchi hizo mbili.
Kupitia majadiliano na hatua za ufuatiliaji wa fursa zilizobainishwa, Tanzania inalenga kuimarisha nafasi yake kama eneo lenye fursa za uwekezaji, huku ushirikiano na sekta binafsi ya Uturuki ukitarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kibiashara.

