Dar es Salaam. Tanzania na Uturuki zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia sekta binafsi, huku Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Viwanda ya Uturuki (MÜSİAD) zikieleza utayari wa kushirikiana katika uwekezaji wa kimkakati, uendelezaji wa mnyororo wa thamani na upanuzi wa biashara baina ya nchi hizo mbili.

Hatua hiyo imefuatia kikao kilichoratibiwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kilichowakutanisha viongozi wa taasisi hizo mbili, wawakilishi wa Serikali na wafanyabiashara kutoka Uturuki, jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kililenga kuweka msingi wa ushirikiano wenye tija kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki, hususan katika sekta za kilimo, nguo, miundombinu na teknolojia, ambazo zinatoa fursa za uwekezaji na kukuza biashara.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Deogratius Massawe, alisema Uturuki ni mshirika wa kimkakati wa Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa sekta binafsi ili kuongeza fursa za uwekezaji na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Alieleza kuwa ushirikiano huo unakuja wakati Tanzania inajiandaa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inahitaji ushiriki madhubuti wa sekta binafsi katika kukuza uzalishaji, biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa MÜSİAD, Bw. Selim Başdemir, alithibitisha utayari wa wanachama wa jumuiya hiyo kushirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania katika kuwekeza na kutekeleza miradi ya kimkakati.

Alisema MÜSİAD, yenye wanachama zaidi ya 14,000 duniani kote, iko tayari kuendeleza ushirikiano na kampuni za ndani kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP), hatua inayoweza kusaidia kuunganisha mitaji, utaalamu na uwezo wa uzalishaji wa pande hizo mbili.

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania na Uturuki zinatarajiwa kuwa na fursa zaidi za kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kuvutia mitaji na kukuza ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo, kwa manufaa ya uchumi wa nchi zote mbili.