Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki umeratibu kambi ya matibabu mahsusi kwa ajili ya afya ya kinywa na meno iliyoendeshwa na Taasisi ya Colors of Africa Association ya Uturuki kwa ushirikiano na TIKA iliyofanyika Tumbatu, Zanzibar. Kambi hiyo ilitoa fursa kwa wananchi kunufaika na huduma mbalimbali za uchunguzi, ushauri wa kitaalamu, huku zaidi ya wananchi 500 wakinufaika na matibabu ya huduma za kibingwa za kinywa na meno.
Vilevile, taasisi hiyo ilitoa vifaa vya matibabu kwenye Kliniki ya Wazazi iliyopo Kichangani ili kuboresha huduma za afya na kusaidia juhudi za Serikali za kuimarisha huduma kwa wananchi.
Kambi hii ni mwendelezo wa ushirikiano mzuri kwenye sekta ya afya kati ya nchi hizi mbili, Tanzania na Uturuki. Ubalozi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaipongeza taasisi hiyo kwa miradi mbalimbali yenye tija ambayo imekuwa ikitekelezwa nchini.


