Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Daniel Sillo amewasili nchini Uturuki kwa ajili ya kumwakilisha Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu katika Mkutano wa 152 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Mkutano huo umepangwa kufanyika Hilton Istanbul Bomonti Hotel kuanzia tarehe 15 hadi 19 Aprili 2026.
Mhe. Sillo baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Istanbul Aprili 13, 2026 amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari. Viongozi wengine walioshiriki mapokezi hayo ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, Geneva, Mhe. Balozi Dkt. Hoyce Temu na Mwakilishi wa Katibu wa Bunge la Tanzania kwenye Mkutano huo Ndg. Daniel Eliufoo.
Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Uturuki Mhe. Recep Tayyip Erdoğan na unawakutanisha Wabunge kutoka nchi 183 wanachama.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa IPU Oktoba 2026 na umepangwa kufanyika jijini Arusha.
Mada mbalimbali zitajadiliwa katika Mkutano huo ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa kimataifa, mabadiliko ya tabianchi, hali ya usalama inayoendelea duniani na Uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja huo.



