Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari, Februari 23, 2026 amekutana na wamiliki wa kampuni za kuzalisha nguo nchini Uturuki katika Makao Makuu ya Jumuiya ya wenye Viwanda na Wafanyabiashara nchini Uturuki (MÜSİAD), Jijini Istanbul.

Mkutano huo, umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uhusiano wa Kidiplomasia wa Jumuiya ya MÜSİAD, Bw. Osman Önügöre pamoja na wadau kutoka kampuni mbalimbali zinazojihusha na sekta ya uzalishaji nguo na uongezaji wa thamani kwenye mnyororo wa zao la pamba.

Balozi Bakari, amewaeleza wadau hao kuwa, Serikali ya Tanzania imeendelea kuboresha uzalishaji wa zao hilo kwa kusambaza mbolea, upatikanaji wa mbegu bora, na kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji ikiwemo Maeneo Maalum ya Kiuchumi mahsusi kama nyenzo muhimu ya kuendeleza viwanda, kukuza uchumi kupitia ajira na kuchochea mauzo nje ya nchi. Hivyo, aliwakaribisha wadau hao kuchangamkia fursa ya uwekezaji wa zao hilo nchini.

Aidha, ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha zao la pamba kwa wingi na limeendelea kuwa zao la kimkakati linalochangia katika kukuza uchumi na kutoa ajira, ambapo kwa mwaka 2025/26 zaidi ya tani 450,000 zinatarajiwa kuzalishwa.

Kufuatia maelezo hayo, wadau hao wamevutiwa na fursa hizo na kuonesha utayari wa kufanya ziara ya kikazi nchini ili kujionea fursa zilizopo ikiwemo soko la pamba, uwekezaji, na ushirikiano na viwanda vya Tanzania ili kuongeza ufanisi kwa maslahi ya pande zote mbili.