Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari ametumia Hafla ya Maadhimisho ya Miaka 62 ya Muungano kuwasihi Watanzania wanaoishi Uturuki kuchangamkia fursa za maendeleo zilizopo ili kuchangia ujenzi wa Taifa kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa mkutano na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Mkoani Konya, nchini Uturuki ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Muungano Aprili 26, 2026.
Mkutano huo ulilenga kudumisha umoja, kuimarisha uhusiano, na kujadili fursa mbalimbali za maendeleo zinazopatika katika nchi hizi mbili.
"Nawahimiza kufanya kazi kwa bidii, kutii sheria na taratibu za nchi mnayoishi, kujisajili katika kanzidata rasmi, na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kudhalilisha heshima na mwenendo mwema wa jamii", Balozi Bakari aliwaambia Watanzania hao.
Mkoa wa Konya ni miongoni mwa mikoa mikubwa nchini Uturuki, ambapo wengi wa Watanzania ni wanafunzi wa elimu ya juu katika fani mbalimbali, huku wengine wakiwa ni wafanyakazi.
Katika juhudi za kuwafikia Watanzania wote katika maeneo mbalimbali ya uwakilishi, Ubalozi umeweka utaratibu wa kuwatembelea na kufanya nao mazungumzo.
Mpango huo ni endelevu, na inatarajiwa kuwa Watanzania wanaoishi katika mikoa mingine nao watafikiwa.
Hafla hii imefanyika wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiendelea kuweka mazingira wezeshi yanayolenga kutambua na kuimarisha mchango wa Diaspora katika shughuli za maendeleo ya Taifa.



