Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari ameshiriki Mkutano wa wadau wa maendeleo ulioandaliwa kwa pamoja baina ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki na Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa kwa Nchi Zinazoendelea (United Nations Technology Bank for the Least Developed Countries - UNTBLDC) uliofanyika tarehe18 Februari 2026, jijini Ankara, Uturuki.

Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi wanachama wa G20 (G20 members) na wadau wa maendeleo ulijadili vipaumbele vya uendelezaji matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na kuzishawishi nchi na wadau hao wa maendeleo kuunga mkono utekelezaji wa miradi hiyo.

Kupitia mpango wa Benki hiyo, Tanzania imechaguliwa kuwa moja ya nchi ya kipaumbele na itanufaika na miradi ya matumizi ya teknolojia katika sekta za kilimo na uchumi wa buluu kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji wenye tija katika mabadiliko ya tabianchi na matumizi bora ya TEHAMA.

Chini ya mpango huo miradi ya kipaumbele inayotarajiwa kutekelezwa nchini ni pamoja na teknolojia ya kuhifadhi mazao ya samaki, mifumo ya ufuatiliaji wa kielektroniki kwa ajili ya uvuvi endelevu wa bahari kuu; na mradi wa kuendeleza kilimo cha mwani kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Katika mkutano huo, Balozi Bakari aliwahahakishia wadau hao utayari wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuwaletea maendeleo wananchi.

Aidha, amewakaribisha wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa kwa Nchi Zinazoendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mchango wa teknolojia katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuchochea uwekezaji wenye tija katika nyanja za teknolojia na maendeleo endelevu yanayozalisha ajira na fursa kwa wananchi.