Ubalozi wa Tanzania – Ankara umetumia fursa ya Jukwaa la Utalii (International Tourism Trade Expo and Congress (TTI İzmir) kutangaza vivutio vya utalii na kuimarisha mawasiliano na wadau mbalimbali ikiwemo kampuni za utalii, usafirishaji, mashirika ya ndege, taasisi za serikali na sekta binafsi.
Jukwaa hilo lililofanyika katika Jiji la Izmir, Uturuki, tarehe 3-5 Desemba 2025, lilihudhuriwa na waendeshaji wa utalii wa kimataifa, wataalamu na watoa huduma, na lilitoa fursa muhimu ya kujadili maendeleo ya utalii ikiwemo utalii endelevu na matumizi ya digitali.
Kongamano hilo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kukuza sekta ya utalii na kuongeza mchango utokanao na sekta hiyo. Ushiriki wa Ubalozi ulilenga kushawishi kampuni na mashirika mbalimbali kushirikiana na wadau wetu nchini Tanzania ili kukuza sekta ya utalii.


