Ubalozi wa Tanzania uliopo nchini Uturuki umefanikisha uratibu wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu itakayofanyika kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dodoma kuanzia tarehe 1-7 Desemba 2025.
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari amewaaga Watalaamu wa afya kutoka Shirika la Can Veren Eller Derneği (Life-Giving Hands Association) la Uturuki katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Istanbul Novemba 29, 2025 kwenda nchini kuanza kambi hiyo.
Ujumbe huo wenye jumla ya watu 10 wakiwemo madaktari na wauguzi unakwenda na vifaa vya kutolea huduma kwa wagonjwa na pia wataendesha mafunzo maalum ya huduma za ubingwa wa juu (super speciality) kwa madaktari wa Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Mafunzo hayo yatahusu masikio, pua na koo (ENT) hususan upasuaji wa mfupa wa sikio (temporal bone surgery), ambao utafanyika katika hospitali hiyo kwa mara ya kwanza.
Shirika la Can Veren Eller lina uzoefu wa muda mrefu wa kuendesha kambi za matibabu na kwa nyakati tofauti limewahi kuendesha kambi za matibabu Zanzibar, mwezi Februari 2024 na Aprili 2025. Hivyo, ziara yao BMH ni mwendelezo wa ushirikiano mzuri ambao umekuwepo baina ya nchi yetu na shirika hilo katika sekta ya afya.
Balozi Bakari amesifu Shirika hilo kwa kuichagua Tanzania kama nchi ya kimkakati kutoa huduma za uchunguzi na matibu kwa wananchi na amewahakikishia dhamira njema ya Serikali ya kushirikiana na wadau mbalimbali ili kunufaika na fursa zenye maslahi kwa nchi yetu katika sekta ya afya, ikizingatiwa kwamba Uturuki inafanya vizuri kwenye sekta hiyo.

