Istanbul, Septemba 8, 2025 – Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mhe. Iddi Seif Bakari, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki, ulitembelea Chemba ya Wafanyabiashara ya Istanbul (Istanbul Chamber of Commerce) na kufanya mazungumzo na Ndg. Ahmet Özer, Makamu wa Rais wa Jumuiya hiyo. Taasisi kutoka Tanzania zilizoshiriki ziara hiyo ni Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha biashara na uwekezaji ili kuweka msukumo wenye tija, kuongeza wigo wa fursa za ushirikiano wa kimkakati na kujadili mwenendo wa biashara baina ya nchi hizi mbili. Lengo ni kukuza biashara na kufikia Dola za Marekani Bilioni Moja (1 billion USD).
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi, aliwasilisha fursa za Baisahara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania kwenye sekta za madini, kilimo, ufugaji, utalii, na miundombinu na kukaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uturuki kuzitumia. Aidha, Chemba ya Wafanyabiashara ya Uturuki ilipongeza ushirikiano mzuri wa biashara uliopo na Tanzania. Wakati wa mazungumzo hayo, Ndg. Özer na ujumbe wake waliarifu kwamba Uturuki imekuwa ikifanya biashara na nchi yetu hususani katika bidhaa mazao na matunda na ingependa kuona biashara kati ya nchi hizi mbili inakua zaidi katika sekta nyingine. Pamoja na hayo, alibainisha utayari wa kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuongeza kiwango hicho cha biashara kwa maslahi ya pande zote mbili. Sambamba na hilo, alieleza dhamira ya chemba za Tanzania na Uturuki kushirikiana kwa karibu ili kukuza sekta ya biashara na uwekezaji. Kabla ya kuhitimisha mazungumzo hayo, ujumbe wa Tanzania ulitoa mwaliko kwa wafanyabiashara kutoka Uturuki kuja na kutembelea nchini Tanzania ili kukutana na wafanyabiashara wenzao kwa ajili ya kubadilishana fursa na taarifa katika sekta mbalimbali za kimkakati.
Ziara hii inajiri wakati ambapo Tanzania na Uturuki zinatarajia kukamilisha utiaji saini wa Makubaliano ya Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili na Makubaliano ya kuanzisha Kamati ya Biashara ya Pamoja kati ya Tanzania na Uturuki ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuchochoea mazingira mazuri ya uwekezaji. Tanzania imejidhatiti kutumia vema fursa ya ushirikiano huo kuimarisha biashara na kuvutia zaidi wafanyabiashara kutoka Uturuki na kuwekeza nchini Tanzania, sambamba na Watanzania kwenda Uturuki kuuza bidhaa za Tanzania kwenye soko la nchi hiyo.