Ubalozi wa Tanzania uliopo Ankara, Uturuki, umeratibu kwa mafanikio ziara ya Madaktari kutoka Shirika la Can Veren Eller la nchini Uturuki kupitia ushirikiano na TIKA ambao wanaendesha kambi ya matibabu kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), jijini Dodoma iliyoanza tangu tarehe 30 Agosti 2026 na kambi hiyo inaendelea.
Ziara hiyo inahusisha madaktari bingwa kutoka Uturuki waliobobea katika magonjwa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na njia ya mkojo, ubongo, mfumo wa chakula na uti wa mgongo. Kupitia kambi hiyo wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya BMH wamefanyiwa uchunguzi na upasuaji mkubwa kwa njia ya matundu katika mfumo wa chakula na mfumo wa mkojo. Upasuaji huo umefanikiwa kwa ushirikiano kati ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na madaktari wa Uturuki, na kwa mara ya kwanza wamefanikisha kufanya upasuaji mkubwa kwa njia ya matundu katika mfumo wa chakula na mfumo wa mkojo. Vilevile, kambi hiyo imechangia kuimarisha ujuzi na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa hospitali hiyo katika kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ziara hii ni utekelezaji wa mkakati wa Ubalozi wa kuimarisha diplomasia ya afya kati ya Tanzania na Uturuki, ili kuwezesha hizi mbili kunufaika na fursa za ushirikiano kwenye sekta ya afya, katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujuzi, matibabu, vifaa na teknolojia.




