Mhe. Balozi Iddi Seif Bakari, Septemba 4, 2025, amepokea ujumbe wa Tanzania, ukijumuisha Wakuu wa Taasisi na Wataalamu kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali ambao upo Istanbul, Uturuki kwa ziara ya kikazi. Ujumbe huo umekuja kushiriki kwenye Mkutano wa Kimataifa wa mazao ya Karanga na Ufuta (World Sesame & Peanut Conference) kuanzia tarehe 5 - 7 Septemba 2025, Istanbul, Uturuki, ambao unahusisha mataifa mbalimbali, ikiwemo Tanzania. Ujumbe huo unaongozwa na Ndg. Sempeho Manongi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara, Wizara ya Viwanda na Biashara, akiongozana na Wakuu wa Taasisi ikiwemo Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC).
Ujumbe huo ukiwa nchini Uturuki utatumia fursa ya mkutano huo kimkakati kujadili maendeleo ya uzalishaji wa ufuta na mazao mengine yenye tija kwa nchi yetu na kuelezea hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya kilimo nchini. Sambamba na hilo, Ujumbe huo pia utafanya mikutano ya pembezoni na kampuni za ufuta na kutembelea viwanda vikubwa vilivyopo Uturuki vinavyochakata zao la ufuta ili kukuza mtandao wa soko, kujifunza ubunifu, teknolojia na kubadilishana uzoefu na washiriki kutoka mataifa mbalimbali yanayolima ufuta kwa wingi pamoja na wanunuzi wa zao hilo.
Katika kuelekea mkutano huo, Balozi Bakari ameelezea mkakati wa Ubalozi wa kukuza biashara kati ya nchi hizi mbili ikiwa ni utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa kuongeza kiwango cha bidhaa za Tanzania zinazoingia kwenye soko la Uturuki ili kuimarisha urari wa biashara na kufungua fursa zaidi za ushirikiano.