Tarehe 14 Mei 2025, Ubalozi ulitembelewa na Bi. Federica Falomi, Mkuu wa Programu (Head of Programme) wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Teknolojia linaloshughulikia nchi zenye uchumi wa chini (UN Technology Bank for the Least Developed Countries) lenye ofisi zake nchini jijini Istanbul, Uturuki. Ujumbe huo ulifanya mazungumzo na Balozi Iddi Seif Bakari ambapo wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Shirika hilo.
Balozi amelipongeza Shirika hilo kwa utekelezaji wa shughuli zake nchini Tanzania ambazo zina mchango chanya katika maendeleo ya teknolojia, uchumi wa buluu, kilimo na mazingira. Vilevile, amekaribisha Shirika hilo kuendelea kushirikiana na sekta za Tanzania katika kuibua maeneo mengine ya ushirikiano yenye maslahi kwa Taifa letu.