Katika kuendeleza jitihada za kuvutia wawekezaji nchini Tanzania, tarehe 14 Mei 2025, Mhe. Iddi Seif Bakari, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki alifanya mazungumzo na wawakilishi wa kampuni ya Alp24 ya nchini Uturuki. Ujumbe wa Kampuni hiyo uliongozwa na Bi. Zeynep Gürkaş, Mkuu wa Uhusiano wa Kimataifa ambaye aliambatana na Bi. Noyan Koval, Head of Business Operations. Wawakilishi hao walifika Ubalozini kwa lengo la kujitambulisha na kuelezea dhamira ya kampuni hiyo kufanya kuwekeza nchini Tanzania kwenye sekta ya nishati ikiwemo kuchakata na kusindika gesi asilia na miradi ya nishati jadidifu.

Kwa upande wake Balozi amesifu kampuni hiyo kwa kuichagua Tanzania kama nchi ya kimkakati kwa uwekezaji huo. Aidha, ameikaribisha kampuni hiyo na kuihakikishia utayari wa Ubalozi katika kuinganisha na sekta zinazohusika nchini Tanzania ili kufanya nao majadiliano ya kina kwa lengo la kufanikisha uwekezaji huo