Istanbul, tarehe 5 Septemba 2025, Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Kongamano la Dunia la Ufuta na Karanga nchini Uturuki, kwa nyakati tofauti ulifanya mazungumzo na Kampuni za TANIŞ Processjng Tech. na AKY Technology za nchini Uturuki. Kupitia vikao hivyo ujumbe huo ulieleza mikakati ya Serikali ya kuendeleza sekta ya kilimo na azma ya kuvutia wawekezaji kutoka Uturuki kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yanayolimwa Tanzania ikiwemo ufuta, karanga na mengine, ili kukuza uchumi wa wakulima na nchi kwa ujumla. Vilevile, vikao hivyo vilijadili fursa ya kukuza mtandao wa masoko wa mazao kutoka Tanzania. Sambamba na hilo, vikao hivyo vilitumika kujifunza maendeleo ya teknolojia ya viwanda na kubadilishana uzoefu ili kuimarisha mnyororo wa thamani, kuongeza tija na ushindani wa nchi yetu katika masoko ya ndani na nje.
Kampuni hizo kutoka Uturuki zinajihusisha na ununuzi wa mazao, uchakataji na uzalishaji wa mashine za kuongeza thamani ya mazao. Kampuni hizo pia zimevutiwa na sekta ya kilimo ya Tanzania na zilionesha utayari wa kushirikiana na nchi yetu katika kuendeleza sekta hiyo kupitia ununuzi wa mazao, uwekezaji na uhaulishaji wa teknolojia.
Aidha, ujumbe wa Tanzania umezialika kampuni na wafanyabiashara kutoka Uturuki kufanya ziara za kikazi nchini ikiwemo kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Saba Saba ambayo hufanyika kila mwaka ili kujionea fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini. Mikutano hii ya kibiashara ni fursa kwa nchi hizi mbili kujadili na kuimarisha ushirikiano wenye maslahi katika sekta za kiuchumi zenye mchango chanya katika maendeleo ya nchi yetu.