Tanzania imeshiriki kwenye Kongamano la Kimataifa la Ufuta na Karanga ambalo lililofanyika jijini Istanbul, Uturuki kuanzia tarehe 5-7 Septemba 2025. Kongamano hilo lilijumuisha mataifa yanayolima mazao ya Ufuta na Karanga, wanunuzi na wazalishaji wa zana za kilimo.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Kongamano hilo uliongozwa na Ndg. Sempeho Manongi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara katika Wizara ya Viwanda na Biashara, ambaye aliambatana na washiriki kutoka Mamlaka ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX). Kupitia kongamanao hilo, Ujumbe wa Tanzania ulielezea hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kukuza uzalishaji wa zao la Ufuta na mazao mengine ili kuinua uchumi wa wakulima na nchi kwa ujumla. Vilevile, ujumbe huo ulishiriki mijadala na mikutano ya pembezoni na kampuni mbalimbali kwa lengo la kuimarisha mtandao wa masoko, kuvutia wanunuzi wa mazao, wawekezaji na teknolojia ya kisasa ili kuongeza tija ya mazao yetu.
Kwa kutambua umuhimu wa kilimo cha ufuta kiuchumi, ujumbe huo ulifanya majadiliano ya kina na kampuni za ufuta na wafanyabiashara wa zao hilo kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kunadi mazao yetu na kushughulikia changamoto za kisekta ili kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa mazao.
Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania inazalisha takribani tani 300,000 za ufuta, kiasi ambacho kinatarajiwa kuendelea kuongezeka. Kwa ujumla ushiriki wa Tanzania kwenye kongamano hilo umetoa fursa ya kuendelea kukuza sekta ya kilimo Kimataifa hususan kupitia wanunuzi wapya, wawekezaji na teknolojia ya kisasa, hatua ambayo itaongeza mauzo ya ufuta nje ya nchi na mapato ya nchi sanjari na kuinua hali ya wakulima wetu.
Ni wazi kwamba ushiriki wa nchi yetu kwenye Kongamano hilo na mchango wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki kwa kuratibu na kufanikisha ziara hiyo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mikakati ya Serikali hususan diplomasia ya uchumi katika kuleta tija na ushindani kwenye sekta za kimkakati ikiwemo kilimo kupitia ushirikiano na mataifa mengine.