Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa kwa nchi zinazoendelea (UNTBLDC), ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Deodat Maharaj, jijini Ankara, Februari 19, 2026.
Kupitia kikao hicho, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo, hususan utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini kupitia uchumi wa buluu, uvuvi na sekta ya kilimo pamoja na jitihada za kushawishi wabia wa maendeleo kuunga mkono utekelezaji wa miradi hiyo.
Sekta hizo zimepewa kipaumbele kutokana na mchango wake wenye tija katika kuzalisha ajira, kuongeza mauzo ya nje na kuimarisha uhusiano muhimu wa sekta mtambuka.
Imeelezwa kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaenda sanjari na mpango mkakati wa Benki hiyo wa mwaka 2025 - 2027, ambao umejikita katika kukuza na kuendeleza teknolojia na ubunifu kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisayansi.
Balozi Bakari amebainisha kuwa Tanzania inaunga mkono azma ya Benki hiyo inayolenga kupanua matumizi ya teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuchagiza maendeleo endelevu kuelekea uchumi unaochochea matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika kufanikisha mipango thabiti ya Serikali kupitia ushirikiano huo.

