Kampuni ya Teknokent (Technopark) kampuni tanzu ya Chuo Kikuu cha Ankara imeonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na Tanzania katika nyanja za teknolojia, utafiti na maendeleo, ubunifu na miradi ya kiuchumi ikiwemo kilimo, ujasiriamali na matumizi ya akili unde (artificial Intelligence).
Hayo yalibainishwa wakati ujumbe wa kampuni hiyo uliongozwa na Meneja Mkuu, Ndg. Mustafa Güray DEĞERLİ ulipokutana na ujumbe wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki Januari 22, 2025.
Ujumbe huo ulieleza dhamira yake ya kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania mwezi Machi 2026 kwa lengo la kukutana na wadau mbalimbali ili kujadiliana maeneo ya ushirikiano na uwekezaji nchini.
Ujumbe huo utakapokuwa nchini unatarajia kufanya mazungumzo na taasisi za Serikali, vyuo vikuu na sekta binafsi ili kubadilishana uzoefu, kuingia makubaliano na kuweka mikakati ya kushirikiana katika matumizi ya teknolojia yenye lengo la kuleta maendeleo nchini.
Ubalozi umeuhakikishia Ujumbe huo utayari wa kuratibu ziara yao nchini Tanzania, huku matarajio ikiwa ni kushawishi uanzishwaji wa Kituo cha Teknolojia (technopark) nchini Tanzania ili kupanua wigo wa matumizi ya teknolojia.

