BALOZI wa Tanzania nchini Uturuki, Prof.Elizabeth Kiondo na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davuto Glu, wameongoza ujio na mapokezi ya wawekezaji wa kampuni saba kubwa nchini Uturuki ambao wamewasili nchini kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali inayohimiza viwanda kuelekea uchumi wa kati.

Wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye maeneo ya viwanda, kilimo na sekta ya umeme, ambapo mikoa ya Dodoma na Simiyu imepewa kipaumbele na wawekezaji hao ambao wataanza zoezi hilo la ujenzi wa viwanda ifikapo Juni 2019.

Akizungumza katika kikao cha pamoja cha wawekezaji hao na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Prof.Elizabeth Kiondo, alisema hatua ya wawekezaji hao kuonesha nia ya kuwekeza nchini inatokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo.

“Wawekezaji hawa wamekuja wakati muafaka kabisa wakati ambao serikali inahimiza uchumi wa viwanda, pia ni kwa sababu serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji, lakini pia tumekuwa tukiwahamasisha waje kuwekeza Tanzania,” alisema.

Alisema bado wana kazi kubwa ya kuhamasisha wawekezaji wa kutoka nchi hiyo kuja Tanzania kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na hivyo ujio wao ni mwanzo tu wa wawekezaji wengine kuja kuangalia fursa zilizopo.

Nae Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Davuto Glu, alisema Tanzania inaelekea kufikia malengo ya kiuchumi hali inayoungwa mkono na serikali ya Uturuki na kuamua kuwahamasisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuwekeza Tanzania.

Mkurugenzi wa uhamasishaji na uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, John Mnali, alizitaka taasisi zinazohusina na maeneo ya uwekezaji kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao ili kurahisisha kazi hiyo kufanywa kwa wakati.