Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari ameipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake "Serengeti Girls U17" kwa ushindi wa kishindo ilioupata, baada ya kuifunga Zambia kwa mikwaju ya penati 4-5. Kufuatia ushindi huo timu hiyo imeibuka mshindi wa tatu, katika mashindano ya Kimataifa ya Kirafiki ya UEFA U18 (WU18 Friendship Cup 2025) ambayo yamehitimishwa leo, jijini Istanbul, Uturuki.

Ikumbukwe kufikia hatua hiyo, timu ya Serengeti Girls ilizifunga timu za Lebanon na Jamaica na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Finland.

Aidha, Katika Mashindano hayo Colombia imekuwa mshindi wa kwanza na Finland mshindi wa pili. Ifahamike kuwa Tanzania na Uturuki zimekuwa na ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo michezo, ambapo baadhi ya vijana wa Tanzania wamekuwa wakicheza kwenye vilabu vya Uturuki. Ubalozi unaendelea na juhudi za kutafuta fursa zaidi kwenye tasnia ya michezo ili kuvutia vijana wengi kuja kucheza kwenye timu za nchini Uturuki.