Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Iddi Seif Bakari, leo Aprili 9, 2025 katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Istanbul, Uturuki amewaaga Madaktari 22 kutoka Shirika la Can Veren Eller ambao wamesafiri kuelekea Zanzibar kwa ziara maalum ya matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.

Madaktari hao wamesafiri na vifaa vya kufanya uchunguzi wa afya na dawa, ambapo watafanya matibabu mbalimbali ikiwemo macho, masikio, wanawake, mfumo wa mkojo pamoja na upasuaji. Kambi husika itatoa huduma za matibabu kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali na watahitimisha ziara yao ifikapo Aprili 20, 2025.

Balozi Iddi amewapongeza madaktari hao kwa utayari wa kutoa huduma za matibabu kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya kukuza ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya afya kati ya Tanzania na Uturuki.

Aidha, Balozi amesema kwamba huduma hizo za matibabu zitaleta tija kijamii kwa kuboresha afya njema na pia  kiuchumi kuimarisha nguvu kazi ya Taifa.

Ziara hii imefanikiwa kwa ushirikiano na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Uturuki (TCT) na wataambatana na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Dkt. Bakari Ramadhani.

  • Mhe. Balozi İddi Seif Bakari akiwa na timu ya madaktari 22 kutoka Shirika la Can Veren Eller