Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili katika jijini Ankara, Uturuki leo tarehe 17 Aprili 2024 kuanza ziara yake ya kitaifa ya siku nne inayofanyika kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mhe. Recep Tayyip Erdogan.
Mara baada ya kuwasili Mhe. Rais Samia alilakiwa na Waziri anayeshughulikia masuala ya Huduma za Jamii na Familia, Mhe. Mahinur Ozdemir Goktaş.
Akiwa nchini Uturuki, Mhe. Rais Samia atapokelewa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Erdogan katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Ankara tarehe 18 Aprili 2024. Viongozi hao pamoja na mambo mengine watashiriki mazungumzo rasmi na dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Mhe. Rais Erdogan kwa heshima ya Mhe. Rais Samia.
Siku hiyohiyo Mhe. Rais Samia atatunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara kutokana na chuo hicho kutambua uongozi wake wa kipekee ambao umeleta mageuzi makubwa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ambayo yameboresha ustawi wa Wtanzania na kuimarisha sifa ya Tanzania ulimwenguni pamoja na kukuza uhusiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine ikiwemo Uturuki.
Mhe. Rais Samia ataondoka Ankara tarehe 19 Aprili 2024 kuelekea Istanbul, mji mkuu wa kibiashara wa Uturuki kwa ajili ya kufungua rasmi Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ambalo litahudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yılmaz.